Dkt. Mwakyembe awaasa vijana kuwa hamna uchawi kwenye michezo
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amewaasa na kuwataka vijana kutumia nguvu zao katika michezo na kufanya mazoezi ila wasije kufikilia kama kuna njia za mkato wala uchawi bali mazoezi ndiyo kila kitu.
Dkt. Mwakyembe amesema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati akikabidhiwa
bendera ya Taifa mbele ya waandishi wa habari na vijana waliyorejea
kushiriki mashindano ya Shirikisho la Michezo Afrika Mashariki (FEASSSA)
yaliyofanyika mwaka huu katika Mji wa Gulu Nchini Uganda ambayo
hushirikisha timu za shule za sekondari za jumuiya ya Afrika Mashariki.
"Nataka kuwadhitibishia Watanzania kwamba tutaenzi daima michezo ya
UMITASHUMTA na UMISETA maana vipaji ndiyo vinapoanzia, niwapongeze sana
vijana kwa kushinda medali nIwatie moyo muendelee ili muweze kushiriki
katika mashindano ya kimataifa yakiwemo Olimpiki, maana nyinyi ndiyo
warithi wa Simbu na wanariadha wengine waliowahi kufanya vyema hapa
nchini," alisema Dkt. Mwakyembe.
Dkt. Mwakyembe akiongea na vijana waliyorejea kushiriki mashindano ya Shirikisho la Michezo Afrika Mashariki (FEASSSA).
Aidha Dkt. Mwakyembe amewaasa vijana hao wasithubutu kutumia njia zisizo
halali ili kushinda, bali wajitume katika mazoezi na wawe na nidhamu ya
hali ya juu kwani michezo ni ajira ya uhakika kwa vijana wengi siyo tu
Tanzania bali hata katika mataifa yote ulimwenguni.
"Tusisikie kabisa kelele za kwamba, unaweza ukafanya hiki au ukatumia
njia za mkato, hakuna mchawi wa michezo zaidi ya mazoezi kwani huwezi
kupata ushindi kwa kupitia njia za kishirikina, haiwezekani kwani hizo
ni hadithi tu za abunuwasi njia pekee ni mazoezi," alisisitiza Dkt.
Mwakyembe.
Vilevile Dkt. Mwakyembe amesema kuwa serikali imejipanga mwaka ujao
itaongeza idadi ya washiriki katika mashindano yatakayofanyika Rwanda na
amewasisitiza vijana pamoja na walimu wa michezo mashuleni kuendelea
kuwalea vijana na kuibua vijana wengi ili kukabiliana na na tatizo la
upungufu wa ajira kwani michezo imekuwa ajira ya uhakika duniani.
Comments
Post a Comment