Ngassa: Simba wasitegemee mteremko kesho
Mchezaji wa Mbeya City, Mrisho Ngassa.
NYOTA wa zamani wa Yanga, Azam FC na Simba ambaye sasa anacheza Mbeya City, Mrisho Ngassa, ameiambia Simba isitegemee mteremko katika mchezo wao wa kesho Jumapili.
Katika mchezo huo namba 72 wa Ligi Kuu Bara, Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Simba kwenye Uwanja wa Sokoine kukiwa na kumbukumbu ya Simba kushinda mabao 2-0 msimu uliopita.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Ngassa alisema hawatakubali kupoteza mechi yoyote watakayoicheza nyumbani ikiwemo hii dhidi ya Simba.
Ngassa alisema, wanaivaa Simba wakiwa tayari wanawafahamu wachezaji wao wote nyota wenye madhara baada ya kuwaona kwenye mechi dhidi ya Yanga.
“Tunawakaribisha Simba huku Mbeya, lakini wanatakiwa kuja kwa tahadhari kubwa kwa kuwa ile Mbeya City waliyoiona kwenye mechi za nyuma siyo hii ya sasa, tumebadilika.
“Mbeya City ya sasa ipo fiti na imekamilika kila sehemu kwani kila sehemu imeboreshwa na tutaingia uwanjani kwa ajili ya kuchukua pointi tatu pekee.
“Hakuna mchezaji tutakayemuhofia Simba na bahati nzuri tuliwaona Uwanja wa Uhuru walipocheza na Yanga, tumewaona wachezaji hatari wanaohitaji uangalizi, kwangu naahidi ushindi,” alisema Ngassa.
Comments
Post a Comment